Rais wa Marekani asema jeshi la Afghanistan linatakiwa kulinda nchi lenyewe
2021-08-11 09:32:00| CRI

Rais Joe Biden wa Marekani amesema jeshi la Afghanistan linatakiwa kulinda nchi lenyewe wakati miji kadhaa ya nchi hiyo ikiangukia  mikononi mwa kundi la Taliban katika siku kadhaa zilizopita.

Rais Biden amesema Marekani imetumia dola trilioni 1 za kimarekani katika miaka 20 iliyopita, na kutoa mafunzo na vifaa vya kisasa kwa askari zaidi ya laki 3 wa Afghanistan. Viongozi wa nchi hiyo wanatakiwa kuungana na kupigania taifa lao wao wenyewe.

Amesema, Marekani itaendelea kutoa uungaji mkono wa anga, chakula, vifaa, mishahara kwa jeshi la Afghanistan, na kuhakikisha jeshi la anga la nchi hiyo linafanya kazi bila matatizo.

Habari nyingine zinasema, kundi la Taliban limetangaza kutwaa mji wa Farah ulioko magharibi mwa Afghanistan.

Shahla Abubaker kutoka baraza la mkoa wa Farah amesema, kikosi cha usalama cha serikali kimerudi nyuma hadi kwenye kituo cha kijeshi kilichopo pembezoni mwa mji wa Farah, ili kuepusha vifo na majeruhi kwa raia wa kawaida.