UM: Maelfu ya watu wakimbia machafuko Afghanistan
2021-08-12 09:05:44| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uratibu wa misaada ya kibinadamu OCHA, imesema makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mapigano yaliyotokea katika sehemu mbalimbali nchini Afghanistan katika wiki iliyopita.

Ofisi hiyo imesema watu hao ni sehemu ya watu karibu laki 3.9 waliopoteza makazi kutokana na mapigano mwaka huu, huku idadi hiyo ikiongezeka kwa kasi tangu mwezi wa Mei. Wengi waliopotea makazi wamekimbilia Kabul na miji mingine mikubwa.

Ofisi hiyo pia imesema wengi wanaokimbilia kwenye mji mkuu sasa wanaishi na familia na marafiki, na wengine wanaishi kwa kuweka kambi kwenye maeneo ya wazi wakikabiliwa na mazingira magumu. Wakimbizi zaidi ya 5,800 wa ndani waliowasili Kabul kutoka Julai 1 hadi Agosti 5 wanahitaji msaada wa chakula na vitu vingine.