Wataalam wa afya ya umma wa Marekani watoa wito kwa rais Biden kutoa chanjo ya COVID-19 kwa nchi nyingine
2021-08-12 10:06:14| cri

Barua iliyoandikwa na wataalam zaidi ya 175 wa afya ya umma wa Marekani, wanasayansi, na viongozi wa vikundi vya kijamii, pamoja na mashirika zaidi ya 50, kwa Rais Joe Biden wa Marekani imechapishwa katika gazeti la Washington Post.

Katika barua hiyo, wataalamu hao wameitaka serikali ya Marekani ichukue hatua haraka kuongeza uzalishaji wa chanjo ya mRNA, na kuuza chanjo kwa nchi za nje kupitia "Mpango wa COVAX" au njia nyingine za usambazaji chanjo za kimataifa, ili kukidhi mahitaji ya kupambana na janga la virusi vya Corona na kuzuia kuibuka kwa virusi hatari zaidi vinavyobadili.

Awali gazeti hilo lilikadiria kuwa jumla ya chanjo za COVID-19 zilizohifadhiwa na serikali ya Marekani zinatosha kutoa dozi kwa watu milioni 750, wakati idadi ya watu wazima nchini humo ni milioni 260. Wakati idadi kubwa ya chanjo nchini Marekani zikiwa hazitumiki, nchi nyingi duniani zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo.

Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika zinaonyesha kuwa, asilimia karibu 1.56 tu ya idadi ya watu barani humo ndio wamepata chanjo kamili ya COVID-19.