Wataalamu wa afya ya umma wa Marekani watoa barua ya pamoja kuihimiza serikali kuuza chanjo ya COVID-19 kwa nchi za nje
2021-08-12 09:06:20| CRI

Wataalamu wa afya ya umma, wanasayansi na viongozi wa asasi za kijamii zaidi ya 175 na mashirika zaidi ya 50 nchini Marekani wameandika barua ya pamoja kwa rais Joe Biden, wakiitaka serikali kuchukua mara moja hatua kupanua uzalishaji wa chanjo ya COVID-19 ya aina ya mRNA na kuuza chanjo hiyo kwa mpango wa chanjo wa COVAX na mifumo mingine ya ugavi wa chanjo ya kimataifa, ili kukidhi mahitaji ya kupambana na janga la Corona duniani na kuzuia kuibuka kwa virusi vipya vyenye hatari zaidi.

Barua hiyo iliyotolewa kwenye gazeti la Washington Post la Marekani imesema, kuibuka kwa virusi vipya vya Delta kumesababisha ongezeko la kasi la wagonjwa katika sehemu mbalimbali duniani, ikionesha tishio linaloletwa na virusi vipya kwa mafanikio yaliyopatikana Marekani na katika nchi nyingine duniani kwenye mapambano dhidi ya janga hilo.

Barua pia imesema Marekani inatakiwa kuongeza uzalishaji wa chanjo ya mRNA ili kutoa chanjo kwa watu bilioni 4 kabla ya mwishoni mwa mwaka huu, huku ikitumia njia ya kuhamisha teknolojia na kutoa fedha kuwezesha kuongezeka zaidi kwa uzalishaji wa chanjo kote duniani.