Marekani yatuma vikosi kwenye uwanja wa ndege wa Kabul kusaidia kuondoka kwa wafanyakazi wa ubalozi
2021-08-13 09:04:04| CRI

Marekani imesema itatuma maelfu ya wanajeshi kwenye uwanja wa ndege wa Kabul ili kuwasaidia wafanyakazi wa ubalozi wake kuondoka wakati hali ya usalama nchini Afghanistan inaendelea kuzorota.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ned Price amewaambia wanahabari kuwa wanaondoa raia wa Marekani kutoka Kabul kufuatia hali ya usalama kuzidi kuzorota, na pia watapunguza wafanyakazi wa ubalozi nchini humo katika wiki kadhaa zijazo.

Bw. Price amesema ubalozi huo bado unafanya kazi, na Marekani inapanga kuendelea na kazi za kidiplomasia nchini humo. Mapema siku hiyo, Ubalozi huo uliwahimiza raia wa Marekani kuondoka Afghanistan mara moja.