Idadi ya vifo kutokana na mafuriko nchini Uturuki yafikia 62
2021-08-16 08:32:40| CRI

Mamlaka ya Kudhibiti Majanga na Masuala ya Dharura nchini Uturuki imesema, idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo katika kanda ya Bahari Nyeusi nchini humo imeongezeka na kufikia 62.

Mamlaka hiyo imesema, mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa yaliikumba kanda ya Bahari Nyeusi kaskazini mwa Uturuki jumatano na kusababisha vifo vya watu 52 katika mkoa wa Kastamonu, huku watu wengine tisa wakifariki katika mkoa wa Sinop na mmoja mkoani Bartin.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Suleyman Soylu amesema, kazi ya uokoaji bado inaendelea katika mikoa hiyo mitatu, huku watu 77 bado hawajulikani walipo.

Mvua kubwa zilizonyesha katika kanda ya Bahari Nyeusi kuanzia wiki iliyopita zimesababisha mafuriko yaliyoharibu nyumba, kubomoa madaraja na kusababisha umeme kukatika katika kanda hiyo.