Marais wa China na Iran watumiana salamu za pongezi kuadhimisha miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi zao
2021-08-16 14:46:49| Cri

Rais Xi Jinping wa China amebadilishana salamu za pongezi na mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi, wakati nchi hizi mbili zikiadhimisha miaka 50 tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi.

Kwenye ujumbe wake Rais Xi amesema tangu pande mbili zianzishe uhusiano wa kibalozi, uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kukua, na urafiki wa jadi umezidi kuimarika. Na tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kimkakati wa pande zote mwaka 2016, kuaminiana kisiasa kati ya pande mbili kumeshuhudia ushirikiano wa kunufaisha kwenye sekta mbalimbali ukiendelea kuongezeka.

Na tangu janga la COVID-19 litokee, pande hizi mbili zimeshirikiana kwenye shida na raha, na kuweka historia nzuri ya ushirikiano kwenye mapambano dhidi ya janga hili.

Rais Raisi amesema Iran na China ni nchi zenye utamaduni wa kale na urafiki kati ya nchi hizi una historia ndefu. Amesema Iran imedhamiria kujenga uhusiano mzuri zaidi kati ya nchi hizo mbili, wakati uhusiano huo unaingia katika muongo wa sita.