Taliban yasema inakusudia kuunda serikali shirikishi nchini Afghanistan
2021-08-18 08:41:53| CRI

Msemaji wa kundi la Taliban Bw. Zabihullah Mujahid amesema kuwa hawataki kuwa na maadui wowote wa ndani au wa nje, na wapanga kuunda serikali ya umoja nchini Afghanistan.

Kwenye mkutano wa kwanza na wanahabari tangu kundi la Taliban litwae udhibiti wa sehemu kubwa ya Afghanistan, Bw. Mujahid amesema wanataka kuwa na uhusiano mzuri na kila mtu, ili kuendeleza uchumi wa nchi hiyo na kufanikiwa. Amesema Afghanistan itakuwa na serikali ya kiislamu yenye nguvu na hakuna wanasiasa watakaopuuzwa katika serikali mpya.

Alisema pia Taliban itawaruhusu wanawake kufanya kazi na kusoma kwa kufuata sheria ya Kiislamu, na watapewa haki zote ndani ya kanuni za Kiislamu, kwa kuwa wanawake ni sehemu muhimu ya jamii.

Katika hatua nyingine, mkuu wa kisiasa wa Taliban Mullah Abdul Ghani Baradar amerudi Afghanistan kutoka Qatar, na ujumbe wake umewasili Kandahar kusini mwa nchi hiyo.