Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa mwito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa nchini Ethiopia
2021-08-20 08:27:44| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres ametoa mwito wa kusitishwa uhasama na kuanza kwa mazungumzo ya kisiasa nchini Ethiopia.

Bw. Guterres amesema watu wa Ethiopia wameteseka sana, hali ya kibinadamu nchini humo ni mbaya na mamilioni ya watu wanahitaji msaada. Miundombinu imeharibiwa, na kuna habari za wanawake kufanyiwa ukatili.

Akiongea jana tarehe 19 Agosti kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ubinadamu, Bw Guterres amesisitiza kuwa hakuna suluhisho la kijeshi la mgogoro wa Ethiopia, na ni muhimu kulinda umoja na utulivu wa Ethiopia, ambayo ni muhimu kwenye kanda yake na zaidi ya hapo.

Amehimiza mapambano yasitishwe, misaada ya kibinadamu isafirishwe bila vikwazo, na kuanza kwa mazungumzo ili kutafuta suluhisho la msukosuko.