Rais wa Iran ataka Marekani iondoe vikwazo
2021-08-23 11:55:48| CRI

Rais Ebrahim Raisi wa Iran ameitaka Marekani ijibu hoja ya jumuiya ya kimataifa ya kwanini ilijitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran bila ya kutekeleza wajibu wake.

Rais Raisi amesema hayo alipokutana na waziri wa mambo ya nje wa Japan Bw. Toshimitsu Motegi mjini Tehran. Hata hivyo amesema Iran inakubali kuendelea kushiriki kwenye mazungumzo kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran lakini Marekani haina sababu ya kuendelea na vikwazo vyake dhidi ya wananchi wa Iran.

Rais huyo pia amesisitiza kuwa masuala ya Afghanistan yanapaswa kuamuliwa na wananchi wa Afghanistan na kwamba madhara yaliyosababishwa na uingiliaji wa nje yameendelea kwa muda mrefu na uwepo wa Marekani hauleti usalama, bali unaleta vitisho.