Raia 19 wauawa kwenye shambulizi nchini Niger
2021-08-23 11:51:13| CRI

Wizara ya mambo ya ndani na usalama wa Taifa imetangaza kwamba raia 19 wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa Ijumaa kwenye shambulizi lililofanywa na watu wenye silaha katika kijiji cha Tem, kilichopo Anzourou, magharibi mwa mkoa wa Tillabery nchini Niger.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, shambulizi hilo lililofanywa na watu wasiojulikana ambao wamekwenda kwa miguu na kuwalenga raia lilitokea Ijumaa saa 3 usiku kwa saa za huko wakati watu wanaendelea na sala. Wizara hiyo imeendelea kusema kwamba wameimarisha usalama kwenye eneo hilo na uchunguzi unaendelea ili kuwapata wahusika wa vitendo hivyo vya jinai na uwoga.

Mkoa huo katika siku za karibuni umekuwa ukishuhudia mashambulizi yakiongezeka dhidi ya vikosi vya serikali na raia, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulizi hayo ya mara kwa mara na kueleza wasiwasi wake juu ya matokeo yake ya hali ya kibinadamu katika eneo hilo.