Maafisa watatu wa polisi wauawa na mtu mwenye silaha nchini Tanzania
2021-08-26 10:34:31| CRI

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania jana alithibitisha mauaji ya polisi watatu na mlinzi mmoja kutoka kampuni binafsi ya usalama yaliyofanywa na mtu mwenye silaha katika majibizano ya risasi.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia alitoa salamu za rambirambi kwa kikosi cha polisi cha Tanzania na kusema wahanga hao wanne waliuawa wakati waliposhambuliwa na mtu mwenye silaha kwenye daraja la Selander lililoko barabara ya Ali Hassan Mwinyi mjini Dar es Salaam. Ameongeza kuwa mshambuliaji huyo amedhibitiwa, na kuiagiza polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Simon Sirro amesema mshambuliaji huyo ameuawa na polisi na kazi ya uchunguzi inafanyika ili kuthibitisha uraia na madhumuni yake.

Shambulizi hilo lilitokea muda mfupi tu baada ya rais Samia kuhutubia maafisa wakuu waandamizi wa polisi na kuwataka kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kuvuka mpaka, ukiwemo ugaidi na usafirishaji wa dawa za kulevya.