Marekani yashauriwa kuwaalika wataalamu wa WHO kuchunguza chanzo cha virusi kwenye Fort Detrick na UNC
2021-08-26 10:38:06| CRI

Marekani imetakiwa kutolifanya suala la kutafuta chanzo cha virusi vya Corona kuwa la kisiasa, na kushauriwa kuwaalika wataalamu wa Shirika la Afya Duniani WHO kuanza uchunguzi kwenye maabara yake ya Fort Detrick na Chuo Kikuu cha North Carolina (UNC) ili kujua chanzo cha virusi, kama inashikilia nadharia yake ya virusi kuvuja kutoka kwenye maabara.

Wito huo umetolewa na msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin jana Jumatano kwenye mkutano na wanahabari, baada ya mjumbe wa kudumu wa China katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Geneva na mashirika mengine ya kimataifa huko Uswisi kumuandikia Mkurugenzi Mkuu wa WHO kuhusu Fort Detrick na UNC, pamoja na barua ya wazi iliyosainiwa na wanamtandao ikitaka kufanyika uchunguzi kwenye maabara hiyo.

Wang amesema msimamo wa China kwenye kutafuta chanzo cha virusi duniani uko wazi kabisa kwamba suala hilo lipo kwenye msingi wa kisayansi, na China siku zote itaunga mkono na kuendelea kushiriki kwenye kutafuta chanzo cha virusi chini ya msingi wa kisayansi.