Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limetangaza mpango wa kudhamini masomo kwa vijana wanawake 25 wa Afrika ili kukuza uwezo wao wa uongozi.
Kwenye taarifa iliyotolewa mjini Nairobi, shirika hilo limesema linaendesha Mpango wa Mafunzo kwa Vijana Wanawake wa Afrika (AfYWL) kwa mara ya pili kwa kushirikiana na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ili kuhimiza usawa wa kijinsia katika uongozi.
Mpango huu unatoa mafunzo kwa walengwa na kukuza uwezo ili kuongeza ushiriki wa vijana wanawake kwenye majukumu ya kufanya maamuzi, na utawaandaa vijana hao kuchangia vyema katika kufanya maamuzi kwa umma, binafsi na kwenye taasisi za kimataifa ndani na nje ya nchi.
Shirika hilo limesema kuwa katika miezi 12 ijayo, wanafunzi hao watapangiwa kwenye makao makuu au ofisi za AUC nchini Ethiopia na New York, au kwenye moja ya ofisi zake za kikanda au nchi.