Uwanja Wa Ndege Kujengwa Eneo La Gatuanyaga
2021-08-30 08:04:01| CRI

Kaunti ya Kiambu nchini Kenya inapanga kujenga uwanja wa ndege katika eneo la Gatuanyaga hivi karibuni.

Mnamo mwaka 2018 kampuni ya matunda ya mananasi ya Delmonte ilitoa ekari 635 kwa Kaunti ya Kiambu, baada ya majadiliano kati ya pande zote mbili.

Makubaliano hayo yalifanyika kati ya mkurugenzi wa kampuni ya Delmonte Bw Stergios Gikaliamoutsas na aliyekuwa gavana wakati huo, Bw Ferdinand Waititu.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema kaunti hiyo itatenga ekari 200 ili kujenga uwanja wa kisasa wa ndege.

Nyoro amesema tayari wameweka mikakati kuona ya kwamba shamba hilo lililotolewa na kampuni ya Delmonte linatumiwa kwa njia inayostahili ili iweze kunufaisha wakazi wote wa Kiambu.

Kampuni hiyo ilitoa kipande hicho mwaka wa 2018 baada ya maelewano ya kuongeza miaka 99 zaidi ili kuendelea na biashara yao hapa nchini.

Kulingana na mpangilio uliokuwepo hapo awali muda wa kampuni hiyo wa kuendelea kufanya biashara yao ulikamilika, na kwa hivyo wakalazimika kurefusha zaidi muda wao.

Hata hivyo, Dkt Nyoro alisema kabla ya jambo lolote kutendeka ni sharti wananchi wahusishwe katika mipango yote itakayoendelea kuhusu ardhi hiyo.