Miili ya wanajeshi wa Marekani waliouawa kwenye mlipuko uliotokea huko Kabul yarudishwa nyumbani
2021-08-30 09:11:11| CRI

Rais Joe Biden wa Marekani jana alihudhuria shughuli ya kupokea miili ya wanajeshi 13 waliouawa nchini Afghanistan katika kituo cha jeshi kwenye jimbo la Delaware.

Rais Biden amehudhuria shughuli hiyo katika kituo cha jeshi la anga la Dover akiambatana na mkewe Bibi Jill Biden, waziri wa mambo ya nje Antony Blinken, waziri wa ulinzi Lloyd Austin na mnadhimu mkuu wa jeshi Mark Milley na maofisa wengine waandamizi wa jeshi la Marekani.

Rais huyo na mkewe wamekutana na jamaa wa wanajeshi hao kabla ya kushuhudia masanduku yaliyofunikwa bendera ya taifa yakibeba miili ya wanajeshi 11 kuwekwa kwenye magari. Kutokana na matakwa ya jamaa, miili ya wanajeshi wengine wawili itapelekwa nyumbani kwa njia ya kibinafsi.

Habari nyingine zinasema jeshi la Marekani limefanya shambulizi la anga dhidi ya gari linalodhaniwa kuwa la kundi la ISIS-K, ambalo lingeweza kuleta tishio kwa uwanja wa ndege wa Kabul.

Msemaji wa Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani Bill Urban ametoa taarifa ikisema, shambulizi hilo limeondoa tishio kubwa linaloletwa na ISIS-K ambalo ni tawi la kundi la IS nchini Afghanistan.