Waziri wa Mambo ya Nje wa China afanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani
2021-08-30 08:49:19| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi jana alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani Antony Blinken , wakibadilishana maoni kuhusu hali ya Afghanistan na uhusiano kati ya China na Marekani.

Kwenye mazungumzo yao Bw. Wang Yi alisema hali ya nchini Afghanistan kimsingi imebadilika, na sasa ni lazima pande zote kufanya mawasiliano na Taliban na kuwaelekeza. Ameihimiza Marekani, kwa msingi wa kuheshimu mamlaka na uhuru wa Afghanistan, kuchukua hatua madhubuti kuisaidia nchi hiyo kupambana na ugaidi na vurugu, badala ya kutumia vigezo viwili au kupambana na ugaidi kwa upendeleo.

Kwa upande wake Bw. Blinken alisema wakati Marekani inakaribia kukamilisha zoezi la kuondoa jeshi lake nchini Afghanistan, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kutoa sauti wazi na ya pamoja ili kuonyesha kuwa jumuiya ya kimataifa inatarajia Taliban kuhakikisha raia wa kigeni wanaondoka kwa usalama na watu wa Afghanistan wanapata msaada wa kibinadamu, na pia wanatakiwa kuhakikisha Afghanistan haitakuwa kimbilio salama kwa ugaidi.