UNICEF latoa wito wa kutotelekeza watoto nchini Afghanistan
2021-08-30 09:12:08| cri

Kutokana na mahitaji ya watoto nchini Afghanistan kuongezeka kwa kasi hivi karibuni, Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa wa kutotelekeza watoto nchini humo.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Asia Kusini Bw. George Laryea-Adjei, amesema watoto wa Afghanistan wameathiriwa vibaya kutokana na kuongezeka kwa mgogoro na kukosekana kwa usalama. Kutokana na hali hiyo watoto wamelazimika kukimbia makazi yao, kukatishwa masomo na kutengwa na marafiki zao, lakini pia wamekosa huduma za kimsingi za afya zinazoweza kuwakinga dhidi ya maradhi mbalimbali kama vile polio na pepopunda na magonjwa mengine.

Inakadiriwa kuwa kama hali hiyo ikiendelea, watoto milioni 1 wenye umri wa chini ya miaka mitano watakabiliwa na utapiamlo. Bw.  Laryea-Adjei ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kutoa misaada zaidi kwa watoto nchini humo, wakati baadhi ya mashirika ya kibinadamu yanafikiria kukatisha misaada kwa Afghanistan.