Somalia yazindua mfumo wa taarifa kuhusu ulinzi wa watoto ili kuwalinda watoto walio hatarini
2021-08-31 09:07:38| CRI

Somalia na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF jana Jumatatu walizindua mfumo wa mtandaoni wa usimamizi wa taarifa kuhusu ulinzi wa watoto (CPIMS+) ili kuimarisha ulinzi wa watoto waishio katika mazingira magumu nchini Somalia.

Waziri wa Wanawake na Maendeleo ya Haki za Binadamu nchini Somalia Hanifa Ibrahim, amesema mfumo huo utaimarisha uwezo wao wa kutambua watoto hao, kuwapatia huduma za kuokoa maisha, na kuwalinda dhidi ya utumikishwaji na udhalilishaji.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa Mogadishu, Bi Ibrahim amesema kuzinduliwa kwa mfumo huo ni hatua muhimu kuelekea kulinda usalama wa watoto walio hatarini, wakiwemo wale waishio mitaani, watoto walionusurika ukatili wa kijinsia, watoto wanaokiuka sheria, watoto wachanga waliotelekezwa na wale wasio na watunzaji.

Kwa mujibu wa UNICEF, watoto milioni 1.8 wako katika hatari ya kukabiliwa na vurugu, kudhalilishwa na kupuuzwa nchini Somalia kutokana na mgogoro unaoendelea, mabadiliko ya tabianchi, umaskini na athari za Uchumi-Jamii za janga la Corona.