Mkuu wa Shirika la Wanawake la UM atoa wito wa kushirikishwa kwa wanawake katika serikali mpya ya Afghanistan
2021-09-01 09:01:23| CRI

Mkuu wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa Bibi Pramila Patten ametoa wito kwa uongozi wa Taliban kuwashirikisha wanawake kwenye serikali mpya ya Afghanistan.

Bibi Patten amesema maendeleo kamili na amani ya Afghanistan vinahitaji ushiriki sawa na wa maana wa wanawake kwenye nyanja zote, ikiwemo maisha ya umma na ya kisiasa. Ushiriki kamili wa wanawake ni muhimu sio tu kwa uwezeshaji wao, bali pia kwa maendeleo ya jamii kwa ujumla. Amesema uongozi wa Taliban unatakiwa kuchukua hatua madhubuti kuwashirikisha wanawake kwenye kutoa maamuzi katika ngazi zote, kitaifa na kimataifa, ili waweze kuendelea kutoa mchango kwa malengo ya usawa, maendeleo na amani.

Bibi Patten pia ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kudumisha ufuatiliaji na hatua ili kuhakikisha haki za wanawake zinalindwa ipaswavyo, na pia amesisitiza umuhimu wa kulinda haki za binadamu, ikiwemo haki za wanawake, na kuhamasisha pande zote kutafuta suluhu shirikishi ya kisiasa inayopatikana kwa njia ya mazungumzo ambayo inahakikisha uwakilishi wa wanawake ulio kamili, wenye usawa na wa maana.