China yaitaka Marekani kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona na utafutaji wa chanzo chake
2021-09-07 13:43:29| cri

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Wang Wenbin amesema, China inaitaka Marekani kusikiliza sauti zenye mantiki za jumuiya ya kimataifa na kuwa muungaji mkono badala ya mharibifu wa ushirikiano katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19.

Bw. Wang amesema hayo wakati akizungumzia kuhusu hoja ya mkuu wa kamati ya COVID-19 ya Jarida la The Lancet Jeffrey Sachs.

Sachs alisema, dunia nzima haijatoa jibu la kutosha kwa maambukizi hayo, na moja kati ya masuala makuu ya kijiografia ni kwamba Marekani imeshindwa kushirikiana na China kutafuta suluhisho la dunia nzima. Pia amesema, Marekani inatakiwa kujifunza njia nzuri za kushirikiana na China kuliko kujaribu kulazimisha nchi nyingine kukubali matakwa yake.

Bw. Wang amesisitiza kuwa jibu la COVID-19 na utafiti wa chanzo cha virusi hivyo vinahitaji mshikamano, ushirikiano na moyo wa kisayansi. Lakini baadhi ya wamarekani wamejaribu mara kwa mara kulifanya suala la kutafuta chanzo cha virusi kuwa la kisiasa katika pande zote mbili na kuhamisha lawama dhidi ya mwitikio wao mbaya.