Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” lasaidia Afrika kuboresha miundombinu ili kupata maendeleo
2021-09-07 14:42:19| CRI

Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” lasaidia Afrika kuboresha miundombinu ili kupata maendeleo_fororder_VCG111104381636

Huu ni mwaka wa nane tangu China itoe pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Katika kipindi hicho, ujenzi wa miradi ya ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika kutokana na pendekezo hilo umepamba moto, na kusaidia nchi za Afrika kuboresha miundombinu ili kupata maendeleo ya uchumi.

Hali duni ya miundombinu ni changamoto kubwa zaidi inayokabili nchi za Afrika katika mchakato wao wa kujiendeleza. Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Afrika inasema, changamoto hiyo inapunguza asilimia 2 ya ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika kwa mwaka.

Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” limeleta matumaini mapya kwa Afrika kushinda changamoto hiyo. Hadi sasa pendekezo hilo limeshirikisha nchi 46 za Afria, ambayo zinachukua asilimia 96.3 ya watu, asilimia 96.1 ya ardhi, na asilimia 98.1 ya uchumi barani Afrika. Katika miaka nane iliyopita, kampuni za China imejenga bustani 45 za viwanda katika nchi 16 za Afrika, viwanda 56 vya kuzalisha umeme katika nchi 23 barani humo, na njia 32 za reli na bandari 33 katika nchi 17 barani Afrika. Miradi hiyo ya miundombinu imekuwa msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi wa nchi hizo.

Kenya ni mshiriki muhimu wa pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Reli ya SGR inayounganisha miji ya Mombasa na Nairobi ilijengwa na kampuni ya China kufuatia pendekezo hilo. Tangu izinduliwe tarehe 31 Mei mwaka 2017, reli hiyo imerahisisha kwa kiasi kikubwa usafiri wa watu na mizigo, ambao awali ulikuwa mgumu na kuchukua muda mrefu njiani. Licha ya hayo, reli hiyo pia imetoa nafasi za ajira karibu elfu 50 kwa Wakenya. Takwimu zinaonesha kuwa, reli hiyo imeongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Kenya kwa asilimia 1.5, na kuwa injini mpya kwa maendeleo ya uchumi.

Mbali na Kenya, reli ya SGR pia imenufaisha nchi nyingine za Afrika Mashariki, zikiwemo Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Uganda. Usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizo zisizo na bandari na nchi za nje kwa njia ya bahari unategemea kwa kiasi kikubwa bandari ya Mombasa ya Kenya. Reli hiyo imezisaidia kuongeza kasi ya usafirishaji na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa. Katibu Mkuu wa Chama tawala nchini Kenya cha Jubilee Raphael Tuju amelipongeza pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kwa kuungana vizuri na malengo ya maendeleo endelevu barani Afrika.

Reli ya SGR ni moja ya miradi mingi ya ushirikiano kati ya China na Afrika kufuatia pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Pendekezo hilo linazisaidia nchi za Afrika kuondoa changamoto ya hali duni ya miundombinu, na kuziwezesha kupata maendeleo endelevu.