UM wawataka viongozi wa Sudan Kusini kumaliza mapigano katika mkoa wa Western Equatoria
2021-09-08 08:49:11| CRI

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini imewataka viongozi wa nchi hiyo kumaliza mvutano katika eneo la Tambura na kanda nzima ya Equatoria Magharibi baada ya kuibuka kwa mapigano mapya.

Mjumbe maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Nicholas Haysom amesema, ukosefu wa usalama una athari kubwa kwa raia, na kuongeza kuwa watu zaidi ya 40,000 wamelazimika kukimbia makazi yao. Amesema ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa katika ngazi ya kitaifa na mitaa kuchukua hatua za dharura kumaliza mvutano huo na kuzileta pamoja kaya zinazopingana ili kuepuka vifo zaidi, uharibifu wa nyumba na maisha ya watu.

Haysom amezitaka pande zinazohusika katika mgogoro huo kumaliza mapigano ili kurejesha usalama, akisema mapigano hayo yanayongeza mahitaji ya msaada wa kibinadamu katika wakati ambao tayari rasilimali zilizopo hazitoshelezi.