Viongozi wa Afrika warejea ahadi yao ya kusimamia ajenda ya usalama wa chakula
2021-09-09 08:53:10| CRI

Wakuu wa nchi na serikali kutoka kanda ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara wamethibitisha tena ahadi yao ya kusimamia ajenda ya usalama wa chakula kama sehemu ya ufufukaji baada ya janga la virusi vya Corona.

Wakizungumza katika mkutano unaoendelea wa Jukwaa la Mageuzi ya Kijani Afrika (AGRF) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya, viongozi hao wamesema mageuzi katika mifumo ya kilimo ili kuboresha chakula, usalama wa lishe na kipato katika maeneo ya vijijini ni muhimu wakati bara hilo likianza kufufuka kutokana na athari za janga la virusi vya Corona.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema, uamuzi wa kutunga sera imara pamoja na uwekezaji katika teknolojia zinazofaa ni ufunguo muhimu katika kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo barani Afrika.

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameema, utayari wa kisiasa ni muhimu katika kufanyia mageuzi sekta ya kilimo barani Afrika inayokabiliwa na changamoto nyingi zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, shinikizo kwa ardhi yenye rutuba, mnyororo ulioharibika wa thamani ya mazao ya kilimo na teknolojia duni.