Xi na Biden wazungumza kwa njia ya simu
2021-09-10 11:53:39| cri

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Marekani Joseph R. Biden leo wamezungumza kwa njia ya simu na kujadiliana kimkakati kwa udhati, kina na mapana juu ya uhusiano wa nchi zao na masuala yanayofuatiliwa nao kwa pamoja.

Kwenye mazungumzo yao, rais Xi Jinping amesema kwa muda mrefu, sera ambayo imechukuliwa na Marekani kuhusu China imeharibu vibaya uhusiano wa nchi hizi, kitu ambacho hakilingani na maslahi ya watu wa China na Marekani na maslahi ya nchi mbalimbali duniani. Amesisitiza kuwa hivi sasa jamii ya kimataifa inakabiliwa na changamoto nyingi za pamoja na China na Marekani zinapaswa kufikiria kwa mapana, kubeba wajibu mkubwa, kutumia ujasiri wa kimkakati na dhamira za kisiasa na kuhimiza uhusiano kati ya China na Marekani urudi kwenye njia sahihi ya utulivu na maendeleo ili kuwanufaisha watu wa nchi hizo mbili na wa dunia nzima.

Rais Xi ameongeza kuwa katika msingi wa kuheshimu ufuatiliaji wa upande mwingine na kushughulikia na kudhibiti tofauti, taasisi husika za nchi hizi zinaweza kuendelea na mawasiliano yao, na kuhimiza uratibu na ushirikiano katika mabadiliko ya tabia nchi, mapambano dhidi ya virusi vya Corona, ufufuaji wa uchumi na masuala mengine makubwa ya kimataifa na ya kikanda, na vilevile kuchimba nguvu za ushirikiano ambazo hazijatumiwa ipasavyo ili kukuza uhusiano wa China na Marekani.

Kwa upande wake, rais Biden amesema uhusiano kati ya Marekani na China ni uhusiano muhimu zaidi wa pande mbili duniani, na nchi mbili hazina haja ya kuzama kwenye mgogoro kwa sababu ya ushindani. Amesisitiza kuwa Marekani haina nia ya kubadilisha sera ya kuwepo kwa China moja tu, na kupenda kufanya majadiliano ya dhati na mazungumzo ya kiujenzi na China ili kuamua maeneo yatakayopewa kipaumbele katika ushirikiano wao, kuepuka kufanya maamuzi kwa makosa na kutokea kwa mgogoro usiotarajiwa, na kufanya uhusiano kati ya Marekani na China urudi kwenye hali ya kawaida.

Marais hao wawili pia wamekubaliana kuendeleza mawasiliano yao na kuviagiza vikosi kazi vyao kuandaa mazingira bora ya kusukuma mbele uhusiano kati ya China na Marekani.