Balozi wa China: Historia itaitendea haki Afghanistan kwa yaliyotokea nchini humo katika miaka 20 iliyopita
2021-09-10 11:52:44| cri

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Geng Shuang amesema historia itaitendea haki Afghanistan kwa yaliyotokea nchini humo katika zaidi ya miaka 20 iliyopita, na kwamba uingiliaji wa kijeshi na siasa za umwamba vimeshindwa.

Balozi Geng Shuang ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, amani na maendeleo ya Afghanistan vimejaa mazonge na kukabiliwa na changamoto nyingi, pande mbalimbali nchini humo zimeshindwa kufikia maafikiano, makundi ya ugaidi hayajatokomezwa na badala yake yamezidi kukua kwa kasi, na watu wa Afghanistan wamepitia mateso na machungu makubwa na kunyimwa maendeleo na heshima, na wameishi maisha magumu katika hali ya umaskini na kukosekana kwa utulivu.

Balozi huyo amesema ni historia tu itakayoitendea haki Afghanistan kwa yaliyotokea nchini humo katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, na kwamba mabadiliko makubwa yaliyotokea hivi karibuni nchini humo yamekumbusha mara nyingine tena kuwa uingiliaji wa kijeshi na siasa za uwamba havikaribishwi, na majaribio ya kupandikiza mifumo ya kigeni na demokrasia katika nchi nyingine hayawezi kufanikiwa.