Mabadiliko ya hali ya hewa ni changamoto kubwa sana kwa haki za binadamu
2021-09-14 09:14:55| cri

Mabadiliko ya hali ya hewa ni changamoto kubwa sana kwa haki za binadamu_fororder_气候变化

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameyataja mabadiliko ya hali ya hewa kama ni “changamoto kubwa zaidi kwa haki za binadamu katika zama za leo”.

Kwenye taarifa yake ya ufunguzi wa kikao cha 48 cha Baraza la Haki za Binadamu kilichoanza jana, Bachelet alisema misukosuko iliyoletwa kwa pamoja na uchafuzi, mabadiliko ya hali ya hewa na anuwai ya viumbe hai inaongeza mara kadhaa vitisho vinavyotokana na migogoro, mivutano, ukosefu wa usawa wa kimuundo, na kuwalazimisha watu kuishi kwenye hali mbaya.

Bibi Bachelet alinukuu ripoti iliyotolewa na jopo la kati ya serikali kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, akisema mabadiliko ya hali ya hewa yameleta madhara makubwa na ya kasi zaidi barani Afrika kuliko sehemu nyingine. Alitoa mfano wa Madagascar kuwa, mamia ya maelfu ya watu walikabiliwa na njaa kali baada ya mvua kutonyesha kwa miaka minne na kupelekea Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP kutoa tahadhari ya “baa la kwanza la njaa lililosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani”.