“Msimu wa kutangaza bidhaa za Afrika kwenye mtandao wa internet” wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika kwa mwaka 2021 umezinduliwa hivi karibuni na utaendelea katika miezi mitatu ijayo. Hili ni tunda la mapema lililopatikana kwa China kutekeleza ahadi yake ya kusaidia Afrika kuhimiza maendeleo ya kidigitali. Katika siku chache zijazo, baadhi ya miradi ya ushirikiano kati ya China na Afrika kama vile ujenzi wa mkonge mkuu wa mawasiliano ya internet na mkutano wa Baraza la Ushirikiano la Mfumo wa Kuongoza Safari wa Beidou kati ya pande hizo mbili pia utakamilishwa au kutekelezwa.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa UNCTAD, nchi za Afrika zinaunga mkono uvumbuzi na uchumi wa kidigitali unaokua kwa kasi, lakini ukosefu wa mpango wazi wa kimkakati unakwamisha maendeleo ya uchumi wa kidigitali. Katika hali hii, kongamanao la maendeleo na ushirikiano la mtandao wa internet kati ya China na Afrika lililofanyika mwishoni mwa mwezi Agosti lilitangaza “mpango wa wenzi wa uvumbuzi wa kidigitali kati ya China na Afrika” na kubainisha kuwa katika miaka mitatu ijayo, China itasaidia kutumia uvumbuzi wa kidigitali “kujenga” mshipa mkuu wa taarifa wa maendeleo ya uchumi na jamii barani Afrika.
Ikikabiliwa na changamoto zinazotokana na janga la virusi vya Corona, dunia inapaswa kushukuru na kukumbatia zaidi aina na matumizi tofauti ya teknolojia ya kidigitali kuliko wakati wowote. Afrika pia inakuwa hivi na kwamba wakati uchumi wake wa jadi unapata pigo kubwa, maendeleo ya kasi ya uchumi wa kidigitali yanapatikana. Katika siku za baadaye, maendeleo ya teknolojia ya digitali na kuinuka kwa uchumi wa kidigitali vitatoa nguvu muhimu kwa ufufuaji wa uchumi wa Afrika, na kusaidia nchi za Afrika kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030. Ndiyo maana, China inatoa mpango wa wenzi wa uvumbuzi wa kidigitali kwa wakati sahihi. Pendekezo hilo lenye hatua kabambe zitakazochukuliwa na China na Afrika kwa pamoja limetolewa katika msingi wa ahadi aliyotoa rais Xi Jinping wa China ya kusaidia Afrika kupanua uchumi wa kidigitali, kujenga miji ya kisasa na mfumo wa 5G kwenye mkutano wa mshikamano wa kupambana na COVID-19 kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana, na kauli iliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi mapema mwaka huu alipofanya ziara barani Afrika, ni kuwa China na Afrika zitajenga kwa pamoja “Afrika ya kidigitali”.
Tangu mwaka 2020, China imeisaidia Afrika kupata maendeleo makubwa katika mtandao wa internet. Mradi wa ujenzi wa mtandao huru wa kwanza wa 5G uliojengwa na makampuni ya China na Afrika Kusini ulikamilika mwaka jana; Kituo cha Data cha taifa cha Senegal kilichojengwa kwa msaada wa kifedha na kiteknolojia wa China kitazinduliwa mwaka huu; jukwaa la biashara ya kimtandao duniani eWTP limesaidia kufikisha bidhaa za Afrika mikononi mwa wateja wa China; mpango wa “mbegu wa baadaye” wa kampuni ya mawasiliano ya simu ya Huawei na “shindano la mashujaa wa biashara wa Afrika” pia vimetoa mchango katika kuandaa vipaji vya mtandao wa internet barani Afrika…… mifano hii inalingana na hatua zilizotajwa na “mpango wa wenzi wa uvumbuzi wa kidigitali kati ya China na Afrika” za kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu ya kidigitali, kukuza uchumi wa kidigitali, kutoa elimu ya kidigitali, kuhudumia umma, kulinda usalama wa kidigitali, na kuanzisha jukwaa la ushirikiano.
Ikilinganishwa na nchi nyingi, nchi za Afrika zinakabiliwa na pengo kubwa la kidigitali, jambo ambalo sio tu halisaidii maendeleo ya muda mrefu ya nchi za Afrika, bali pia kukwamisha juhudi za Afrika kuondoa umaskini. Kujifunza “fikra za kidigitali” ni muhimu kwa Afrika, na kwa kupitia kujenga uhusiano wa kiwenzi na China, nchi za Afrika zinaweza kupunguza gharama za mabadiliko ya kidigitali. Katika ngazi ya taifa, nchi za Afrika zinaweza kulinda thamani na uzoefu wa Afrika kwa kutumia jukwaa jipya la digitali, na pia kutoa sauti kimataifa; na kwenye ngazi ya mtu binafsi, kwa kupitia maendeleo ya kidigitali, kampuni zinaweza kugeuza fikra za digitali kwenye matumizi halisi, kama vile akili bandia na malipo kwa njia ya mtandao, ili kurahisisha maisha ya mtu mmoja mmoja. Ni kwa kufanya hivyo tu, ndipo kujenga “jumuiya yenye hatma ya pamoja kwenye mtandao wa internet kati ya China na Afrika” kunaweza kuwa “wazo kubwa” na pia kutekelezwa kivitendo ipasavyo.