Biden ataka kufanya mazungumzo ya simu na Macron kufuatia mgongano uliotokana na mkataba wa nyambizi
2021-09-21 09:09:12| CRI

Rais Joe Biden wa Marekani anataka kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron, ikiwa ni juhudi ya kupunguza mivutano iliyotokana na mkataba wa nyambizi.

Mgongano ya kidiplomasia uliibuka kati ya Marekani na Ufaransa kufuatia Marekani na Uingereza kutangaza kuwa zitaiunga mkono Australia kuunda nyambizi za nyuklia, zikiipoka Ufaransa mkataba wa kuuza nyambizi 12 za kawaida kwa Australia.

Baada ya kukasirishwa na hatua hiyo ya ghafla bila ya kuarifiwa, Ufaransa iliwarudisha mabalozi wake nchini Marekani na Australia Ijumaa iliyopita.

Ofisa habari wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki amewaambia wanahabari kuwa mazungumzo hayo ya simu yatafanyika katika siku kadhaa zijazo na bado wanaifanyia kazi na kupanga shughuli hiyo.