Wapiganaji 15 wa kundi la al-Shabaab wauawa kwenye pwani ya Kenya
2021-09-28 08:51:25| CRI

Wapiganaji 15 wa kundi la al-Shabaab wameuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa awali kando ya barabara na wapiganaji wa kundi hilo katika eneo kati ya Kiunga na Ishakani, karibu na mpaka wa Kenya na Somalia jumapili iliyopita.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) Esther Wanjiku amethibitisha tukio hilo, akisema hakuna askari wa Jeshi hilo waliokufa ama kujeruhiwa katika tukio hilo. Amesema bomu hilo lilitegwa na timu tofauti ya kundi la al-Shabaab lilikuwa limelenga msafara wa vikosi vya usalama vinavyoendesha operesheni ya usalama ya Linda Boni katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa, operesheni kubwa ya doria zimeanzishwa katika eneo la Msitu wa Boni kwa lengo la kuwaondoa wapiganaji wa kundi la al-Shabaab ambao huenda bado wamejificha katika Msitu huo.