Mtanzania aeleza jinsi China inavyotoa fursa kwa Afrika
2021-09-28 15:14:11| CRI

Mtanzania aeleza jinsi China inavyotoa fursa kwa Afrika_fororder_1

Maonesho ya pili ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika yanafanyika mjini Changsha mkoani Hunan, China, na kuwashirikisha watu mbalimbali kutoka China na Afrika. Katika eneo la mashirika ya Beijing la maonesho hayo, mwafrika mmoja kutoka Tanzania amevutia ufuatiliaji, kwani yeye ni mtia sauti kwenye tamthilia za China kwa lugha ya Kiswahili.

Bw. Alex Herbert kutoka Tanzania aliyesomea kozi ya historia katika Chuo Kikuu, sasa anafanya kazi kama mwigizaji wa sauti nchini China katika Kampuni ya Startimes. Mwaka 2017, kampuni hiyo iliandaa mashindano ya watu wa kutia sauti kwenye tamthilia nchini Tanzania. Alex alishiriki kwenye mashidano na kufanikiwa kuingia fainali, hatimaye aliajiriwa na kampuni hiyo. Hadi sasa ametia sauti kwenye vipindi vingi vya Televisheni vya kampuni hiyo, ikiwemo Amazing Class, Why why why, na Mezani Leo.

Ili kutoa filamu na tamthilia za China kwa watazamaji wa Afrika, tangu mwaka 2016, Kampuni ya Startimes iliandaa mashindano 23 ya uigizaji wa sauti katika nchi tano za Afrika zikiwemo Tanzania, Nigeria, Cote d'Ivoire, Afrika Kusini na Msumbiji, ili kuwachagua watia sauti, na mabingwa watapata nafasi ya kufundishwa na kufanya kazi mjini Beijing kwa miaka miwili.

Alex anafurahia kazi yake hapa Beijing, na anaona fahari sana wakati filamu na tamthilia alizotia sauti zinaoneshwa nchini Tanzania, kwani watu wengi hawafahamu Kichina wala Kiingereza, na kazi yake imewawezesha kujua mambo ya China, na kuhimiza mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Afrika.