Umoja wa Mataifa wazitaka pande zinazopingana nchini Sudan kufikia makubaliano
2021-09-29 09:06:56| cri

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia kipindi cha mpito nchini Sudan (UNITAMS) Volker Perthes amezitaka pande husika kufikia makubaliano na kufanya kazi pamoja ili kutimiza majukumu ya kipindi cha mpito nchini humo.

Perthes amesema hayo jana Jumanne alipokutana na kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa Baraza la Utawala nchini Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan katika ikulu mjini Khartoum. Perthes amepongeza maendeleo makubwa yaliyopatikana nchini Sudan katika miaka miwili iliyopita, na kusema mafanikio hayo ni hatua nzuri kuelekea kutimiza demokrasia, amani, utulivu na haki.

Ameongeza kuwa, ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan inalenga kuwasaidia wananchi wa Sudan na pande zote kutimiza mpito wa kisiasa, kuunga mkono mazungumzo ya amani, kutekeleza Makubaliano ya Amani ya Juba, na kusaidia ujenzi na kuunganisha mihimili ya Amani katika maeneo yaliyoathiriwa na vita.