YouTube kuondoa taarifa zote za kupotosha ambazo zinapinga chanjo
2021-09-30 10:44:21| cri

YouTube imesema itaondoa maudhui yanayoeneza taarifa za kupotosha kuhusu chanjo zote zilizoidhinishwa kwa matumizi, na kupanua marufuku yake kwa madai yote ya uongo yanayotolewa dhidi ya chanjo za COVID-19.

Kampuni hiyo ilisema video ambazo zinasema chanjo ni hatari na zinasababisha usonji, saratani au ugumba ni miongoni mwa zile ambazo zitaondolewa. Sera hiyo inajumuisha kufunga akaunti za watu wanaosambaza taarifa hizo potofu. Youtube imekuwa ikilalamikiwa kwa kutochukua hatua ya kupambana na taarifa za uongo kuhusu afya kwenye tovuti zake.

Mwezi Julai, Rais wa Marekani Joe Biden alisema majukwaa ya mitandao ya kijamii yanawajibika kwa kiasi kikubwa kuwatia watu hofu ya kwenda kuchoma chanjo kutokana na kusambaza taarifa za uongo, na kuyataka kukabliana na tatizo hilo.