Serikali ya China yaandaa tafrija ya kuadhimisha miaka 72 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China
2021-10-01 10:03:47| cri

Serikali ya China jana Alhamis iliandaa tafrija ya kuadhimisha miaka 72 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Rais Xi Jinping na viongozi wengine wa Chama na serikali pamoja na wageni wapatao 500 walihudhuria tafrija hiyo.

Akihutubia katika tafrija hiyo, Waziri mkuu wa China Bw. Li Keqiang amesema mwaka huu China imeadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China CPC. Chini ya uongozi wa CPC, China mpya imepata maendeleo makubwa katika miaka 72 iliyopita, haswa kutimiza lengo la kwanza la Miaka Mia Moja yaani kukamilisha ujenzi wa Jamii yenye Maisha Bora kama ilivyopangwa, na kufungua safari mpya ya kuijenga kwa pande zote China kuwa nchi ya kisasa ya kijamaa.

Habari nyingine zinasema Bw. Li Keqiang siku hiyo pia alikutana na wataalamu wa kigeni waliopata tuzo ya urafiki ya serikali ya China ya mwaka 2020 na 2021. Amesema, China itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, kushiriki kwa kina zaidi kwenye mtandao wa mavumbuzi duniani, kuhimiza ushirikiano na mawasiliano ya kimataifa kwenye fani za teknolojia, wataalamu na miradi, na kuunga mkono wanasayansi wa nchi mbalimbali kufanya utafiti kuhusu changamoto zinazoikabili dunia.