Korea Kaskazini yaamua kufungua laini zote za mawasiliano ya simu na Korea Kusini
2021-10-04 09:44:58| cri

Korea Kaskazini yaamua kufungua laini zote za mawasiliano ya simu na Korea Kusini_fororder_1

Kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), Korea Kaskazini imeamua kufungua laini zote za mawasiliano ya simu na Korea Kusini kuanzia leo Jumatatu saa 3 asubuhi.

Ripoti zimesema uamuzi huo ulitangazwa baada ya ahadi iliyotolewa na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un kwenye hotuba yake ya Alhamis ambayo ameeleza nia yake ya kufungua laini zote za mawasiliano ya simu zilizofungwa kati ya pande hizo mbili, ikiwa kama juhudi za kutimiza matarajio na hamu ya wananchi wote ambao wanataka kuona uhusiano kati ya kaskazini na kusini unarejeshwa. Ripoti hiyo imeongeza kuwa mamlaka ya Korea Kusini inapaswa kufanya juhudi ya kurejesha uhusiano huo na kupanga kazi muhimu ambazo lazima zipewe kipaumbele ili kuleta ustawi mzuri katika siku za mbele, na kutilia maanani maana ya kurejesha tena mawasiliano hayo.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili hauko vizuri tangu mkutano kati ya Korea Kaskazini na Marekani kutofikia makubaliano mapema mwaka 2019. Laini zote za simu kati ya nchi hizo mbili zilifunguliwa mwishoni mwa Julai lakini baada ya wiki mbili Korea Kaskazini ilianza kukataa tena simu za kawaida za Korea Kusini ikipinga mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya Korea Kusini na Marekani.