Siku ya Kuondoa Umasikini Duniani ambayo inaangukia tarehe 17 Oktoba ya kila mwaka, ni siku ambayo watu duniani kote wanapaza sauti zao na kuzitaka serikali na watunga sera kuchukua hatua za kutokomeza umasikini. Hii pia ni siku ya kusisitiza juhudi kwa wale wote wanaoishi kwenye dimbwi la umasikini kupambana na matumizi mabaya ya madaraka na kudai haki zao za kibinadamu. Wanawake na wasichana wanaoishi kwenye umasikini wanakuwa hatarini zaidi kukabiliwa na matukio kama ya ukatili wa kingono na biashara ya binadamu. Na wale wote wanaokumbana na ukatili wa majumbani au wa wapenzi wao huwa wana njia chache za kujikwamua na uhusiano huo, kutokana na ukosefu wa mapato na rasilimali. Hivyo katika kipindi cha leo tutaangalia juhudi za kupunguza umaskini kwa wanawake ni sehemu muhimu ya kutokomeza kabisa umaskini.