WHO lapendekeza kueneza matumizi ya chanjo ya kwanza ya malaria duniani
2021-10-07 10:03:14| CRI

WHO lapendekeza kueneza matumizi ya chanjo ya kwanza ya malaria duniani_fororder_11

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kwamba limependekeza kueneza matumizi ya chanjo ya kwanza ya malaria duniani iitwayo RTS,S/AS01 (RTS,S) kwa watoto wa nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara.

Kwa mujibu wa WHO, chanjo hiyo ni matokeo ya utafiti wa miaka 30 na kuendelezwa na kampuni ya dawa ya Uingereza GlaxoSmithKline (GSK) ikishirikiana na shirika lisilojipatia faida la kimataifa la Mpango wa Teknolojia inayofaa ya Afya (PATH) pamoja na mtandao wa vituo vya utafiti vya Afrika.

WHO imesema mapendekezo yake yanatokana na matokeo kutoka zaidi ya dozi milioni 2.3 za chanjo ambazo zimetolewa kwa zaidi ya watoto laki 8 katika nchi za majaribio ambazo ni Ghana, Kenya na Malawi tangu mwaka 2019. Kwa mujibu wa WHO zaidi ya theluthi mbili ya watoto katika nchi hizo tatu ambao hawakuwa wakilala kwenye vyandarua walinufaika na chanjo hiyo na kupunguza malaria kali kwa asilimia 30.