Viongozi wa UM na nchi mbalimbali watoa wito wa kuimarisha uhifadhi wa bioanuwai duniani
2021-10-13 08:54:07| CRI

Mkutano wa viongozi wa Mkutano wa 15 wa Nchi Zilizosaini Mkataba wa Bioanuwai (COP15) ulifanyika jana mjini Kunming mkoani Yunnan, China, ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres na viongozi wa nchi mbalimbali wametoa wito wa mshikamano zaidi katika kuimarisha uhifadhi wa anuwai ya viumbe duniani.

Akitoa hotuba kwa njia ya video Bw. Guterres ameishukuru China kwa kuitisha na kuandaa mkutano huo wa Kunming na kusukuma mbele “Mfumo wa Bioanuwai Duniani Baada ya Mwaka 2020”. Amesema, mfumo huo unapaswa kujiunga na Makubaliano ya Paris ya Tabianchi na makubaliano mengine ya pande nyingi yanayohusiana na uhifadhi wa misitu, usimamizi wa jangwa na bahari na kuwa nguvu ya pamoja ili kusukuma mbele uhusiano kati ya binadamu na maumbile urudi kwenye njia sahihi.

Marais wa Russia, Misri, Uturuki, Ufaransa na nchi nyingine nyingi pia wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushikamana zaidi katika kutekeleza jukumu la pamoja la binadamu kulinda mazingira ya asili na kuhifadhi anuwai ya viumbe.