Kenya yatarajia kutokomeza malaria kwa kutoa chanjo ya ugonjwa huo
2021-10-15 09:17:17| CRI

Wizara ya Afya ya Kenya imesema chanjo ya Malaria itatolewa kwa wingi nchini humo ili kuongeza juhudi za kutokomeza ugonjwa huo ambao ni chanzo kikuu cha vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito ifikapo mwaka 2030.

Waziri wa afya wa Kenya Bw. Mutahi Kagwe amesema serikali itawekeza katika miundombinu na nguvu kazi ili kupanua upatikanaji wa chanjo ya malaria katika maeneo yanayoathirika zaidi, ikiwa ni sehemu ya mkakati kabambe wa Kenya wa kupambana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa waziri huyo, chanjo hiyo ya malaria ambayo ilitolewa kwanza katika nchi za Kenya, Ghana na Malawi mwaka 2019, imethibitishwa kuwa na ufanisi dhidi ya ugonjwa huo, na mpaka sasa kaunti nane za magharibi mwa Kenya zimekuwa zikitoa chanjo hiyo kwa watoto, hatua ambayo imepunguza kidhahiri maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.