“Vita ya uvumbuzi”dhidi ya China haitafaulu
2021-10-20 15:21:15| cri

“Vita ya biashara” iliyoanzishwa na Marekani haikuweza kurudisha nyumbani kampuni zake kutoka China, “vita ya uvumbuzi” pia haitafaulu_fororder_VCG31N1231336818

 

Waziri wa biashara wa Marekani Gina Raimondo ameviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa nchi hiyo inapaswa kushirikiana na washirika wake wa Ulaya ili kuzuia China kupata teknolojia ya hali ya juu na kupunguza kasi ya maendeleo ya uvumbuzi ya China. Pia ametaja kuwa kanuni za sekta ya teknolojia duniani zinapaswa kutungwa na Marekani na Ulaya kwa pamoja ili kushindana na China.

 

Kauli yake hii wazi ya “kuikandamiza China” imewakumbusha watu kuhusu walichosema rais wa Marekani aliyepita Donald Trump na waziri wake wa mambo ya nje Mike Pompeo walipoanzisha “vita ya biashara” dhidi ya China. Hata hivyo kama Marekani inapanga kuanza “vita” nyingine kuhusu teknolojia na uvumbuzi dhidi ya China, hakika itakuwa kama hali ya “vita ya biashara” iliyoanza miaka michache iliyopita, na Marekani itajiumiza yenyewe.

 

Makala iliyochapishwa hivi karibuni kwenye gazeti la The Washington Post la Marekani imenukuu ripoti ya utafiti iliyotolewa na watafiti Samatha Vortherms na Jiakun Jack Zhang kuwa katikati ya mwaka 2018, ili kuzirudisha nyumbani kampuni za Marekani, serikali iliyoongozwa na Trump ilitoa amri ya kuongeza ushuru kwa bidhaa zilizozalishwa nchini China. Lakini matokeo yameonesha kuwa sera hiyo sio tu imeumiza uchumi wa Marekani, na pia haikuweza kuilazimisha China ibadilishe sera yake ya uchumi.

 

Watafiti wamegundua kuwa ingawa hatua za ushuru za “nipe nikupe” na ushindani mkali zimeongezeka kati ya China na Marekani, kampuni za nchi hizi bado zimedumisha ushirikiano wa kina. Mwaka jana, uwekezaji wa kigeni ulioingia nchini China uliweka rekodi mpya na kufikia dola za kimarekani bilioni 144.4. Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen naye pia alisema, kihalisia wahanga wa hatua ya ushuru ya Marekani ni wanunuzi wa nchi hiyo.

 

Hata hivyo, serikali ya Marekani inayoongozwa na Joe Biden inapanga kuendelea na sera kama hiyo kwa China, na kusambaza “vita” kwenye sekta za biashara na teknolojia kwa pamoja. Katika miaka 10 ya mwanzo ya karne ya 21, serikali ya Marekani na kampuni kubwa za teknolojia za nchi hiyo zilipuuza kampuni za teknolojia za China, na kuona kwa mazoea kuwa teknolojia zao zitaendelea kuwa bora zaidi katika miaka kadhaa na hata miongo kadhaa iliyofuata. Lakini sasa teknolojia bora walizo nazo kampuni za nchi za magharibi zinapungua, hali ambayo imedokezwa na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Marekani katika kupunguza ushawishi wa kampuni za China.

 

Katika macho ya watu wengi, nchi za magharibi zitakuwa na nguvu kubwa ya muda mrefu katika semiconductor, roboti na teknolojia nyingine nyingi za hali ya juu. Lakini halisi ni kuwa sasa China iko mbele katika teknolojia mbalimbali za hali ya juu. Aliyekuwa mkuu wa utafiti wa hisa wa benki ya HSBC kanda ya Asia na Pasifiki William Bratton, hivi karibuni aliandika makala kwenye jarida la Nikkei Asian Review la Japan, akitoa mfano wa sekta ya benki na kusema, benki za nchi za magharibi zimeshindwa kupata mafanikio nchini China, kwani ziko nyumba sana kiteknolojia kuliko benki za China. Siku hizi, katika sekta kama akili bandia, magari yanayotumia umeme, biashara ya mtandao n.k, China inaweza kupimana nguvu na nchi za magharibi, na hata kuzishinda.

 

Pengine mpango wa Marekani wa kushirikisha washirika wa Ulaya kuiwekea China vikwazo vya kiteknolojia unaweza kupunguza kasi ya maendeleo ya teknolojia ya China, lakini kama kuna anayeona hatua hizi zinaweza kuondoa kabisa hamu na uwezo wa China katika uvumbuzi, basi hatimaye atathibitishwa kuwa amekosea.

 

Kwanza China ina mlolongo kamili wa uzalishaji ndani ya nchi ambao unaweza kuunga mkono utekelezaji wa dhamira yake ya muda mrefu. Kwa mujibu wa Shirika la Hakimiliki za Ubunifu Duniani WIPO, mwaka 2020, China iliwasilisha maombi ya hataza 68,720, idadi ambayo iliongezeka kwa asilimia 16 kuliko mwaka 2019. Marekani iliyoshika nafasi ya pili iliwasilisha maombi ya hataza 59,230, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3. Na kampuni ya teknolojia ya China Huawei inayochukuliwa kama ni adui namba moja ya Marekani iliwasilisha hataza 5,464 na kuongoza duniani kwa miaka minne mfululizo.

 

Pili, kwa mujibu wa takwimu rasmi ya China, mwaka 2020 China ilitenga Yuan trilioni 2.4, sawa na dola za kimarekani bilioni 375 kwenye mambo ya utafiti na maendeleo R&D, kiasi ambacho kimechukua asilimia 2.4 ya pato la taifa la mwaka huo, na kukizidi kile cha Marekani kuwa namba moja duniani. China inaweza kutoa teknolojia na huduma za kisasa kwa nchi nyingi na kuongeza fursa za ushirikiano. Kwa hiyo ikizingatiwa faida za kiuchumi, ni vigumu kwa nchi na kampuni za nchi nyingine “kutoichagua China”.

 

Ndiyo maana, sio tu “vita ya biashara” bali pia “vita ya uvumbuzi”, pengine hatua za Marekani za kuipa changamoto China zinaweza kuleta athari mbaya ya muda mfupi, lakini kwa muda mrefu, “juhudi” kama hii itakuwa bure, na pia itasaidia China iinuke kwa haraka zaidi. Cha muhimu zaidi ni kuwa Marekani kuchukulia China kama “adui wa kufikirika” haiwezi kuongeza ushindani wake. China imesisitiza kuwa inapenda kufanya mawasiliano na ushirikiano na Marekani, lakini pia imejiandaa vya kutosha na uwezekano wa kutokea kwa hali mbaya zaidi.