Mkuu wa jeshi la Sudan asema mpasuko katika serikali ya mpito ya Sudan umesababisha uingiliaji wa kijeshi
2021-10-26 09:09:48| cri

Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Sudan ambaye pia ni kamanda mkuu wa majeshi ya Sudan Bw. Abdel Fattah Al-Burhan jana alisema, mpasuko miongoni mwa wenzi wa serikali ya mpito ya Sudan umesababisha uingiliaji wa kijeshi ili kuzuia vurugu nchini humo.

Al-Burhan ametangaza Sudan imeingia katika hali ya dharura, na inavunja Baraza la Utawala na serikali yake, na kuwaondoa wakuu wa mikoa yote kwenye nafasi zao.

Wizara ya utamaduni na habari ya serikali ya mpito ya Sudan jana usiku ilitoa taarifa ikisema, operesheni ya upande mmoja iliyofanywa jana na jeshi la Sudan ni kitendo kisichofuata msingi wa katiba. Taarifa hiyo pia imesema serikali inayoongozwa na Abdalla Hamdok ni serikali halali ya mpito ya Sudan. Hamdok pamoja na mawaziri wa serikali yake sasa wamekamatwa na jeshi la Sudan.