Waziri mkuu wa China ahimiza ushirikiano kati ya China na jumuiya ya ASEAN
2021-10-27 11:14:25| cri

Waziri mkuu wa China Bw. Li Keqiang amesema China itaimarisha urafiki na ushirikiano wa kunufaishana na Jumuiya ya nchi za Asia Kusini Mashariki ASEAN.

Bw. Li amesema hayo kwa njia ya Video wakati akishiriki kwenye mkutano wa 24 wa viongozi wa China na ASEAN.

Bw. Li amesema uhusiano kati ya China na ASEAN umeendelezwa kwa utulivu na kuwa imara, na ushirikiano wenye ufanisi katika sekta mbalimbali unaendelea kusonga mbele. Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 30 tangu uhusiano wa mazungumzo kati ya China na ASEAN kuanzishwa. Katika miaka 30 iliyopita, pande mbili zimeshikilia ushirikiano wa kunufaishana, kuunga mkono mfumo wa pande nyingi, kuhakikisha utulivu wa kikanda na kudumisha ukuaji wa uchumi. Wakati pande mbili zikikabiliwa na athari za COVID-19, China na ASEAN zimesaidiana na kuungana mkono, na kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Bw. Li pia amesema China inapenda kuimarisha ushirikiano wa kirafiki na wa kunufaishana na nchi mbalimbali ikiwemo nchi za ASEAN kupitia ufunguaji mlango.