Mkutano wa G20 watoa wito wa kuhimiza usambazaji wa chanjo za Corona kwa usawa
2021-10-31 11:29:11| Cri

Viongozi wa nchi nyingi na wakurugenzi wa mashirika ya kimataifa walihutubia mkutano wa wakuu wa kundi la nchi 20 (G20) uliofunguliwa tarehe 30 mjini Rome nchini Italia, ambao wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa iimarishe ushirikiano katika kukabiliana na janga la Corona na suala la usambazaji wa chanjo za Corona kwa usawa.

Waziri mkuu wa Italia Bw. Mario Draghi jana amehutubia ufunguzi wa mkutano huo akitoa wito kwa nchi mbalimbali ziimarishe ushirikiano, na kuzitolea nchi maskini zaidi chanjo za Corona na kuhimiza kugawanya chanjo kwa usawa kote duniani.

Rais Vladimir Putin wa Russia ametoa wito kwa Kundi la G20 litatue suala la kukubaliana chanjo na vyeti vya chanjo haraka iwezekanavyo.

Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Boris Johnson amesema kipaumbele cha kazi ya Kundi la G20 ni kuhimiza kugawanya chanjo za Corona kwa usawa haraka kote duniani.

Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya Bw. Charles Michel amesema nchi za Kundi la G20 zinapaswa kuchukua hatua zenye uratibu ili kukabiliana na changamoto kubwa.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Bw. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema uhakikisho wa kugawanya chanjo za Corona kwa usawa unaendana na maslahi mazuri zaidi kwa nchi zote. Ametoa wito kwa Kundi la G20 litoe chanjo haraka kama lilivyoahidi hapo awali, na kuunga mkono kutengeneza chanjo za Corona barani Afrika.