Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Marekani wakutana mjini Rome
2021-11-01 09:08:41| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi amekutana na mwenzake wa Marekani Bw. Antony Blinken huko Rome.

Kwenye mazungumzo yao Bw. Wang Yi amesema katika miaka ya hivi karibuni uhusiano kati ya China na Marekani umeshuka kutokana na Marekani kutekeleza sera za makosa kuhusu China. Uzoefu muhimu uliopatikana katika miaka 40 iliyopita tangu nchi hizo mbili zianzishe uhusiano wa kibalozi, unaonesha kuwa China na Marekani zikishirikiana zitanufaishana, lakini zikipambana zote zitapata hasara. Maoni ya pamoja yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya simu kati ya marais wa China na Marekani, ni kuwa pande hizo mbili zinapaswa kurejesha mazungumzo na kuepuka makabiliano. Amesema kazi muhimu kwa sasa ni kutekeleza kihalisi makubaliano hayo kati ya wakuu wa nchi hizo mbili, na kuweka msingi wa kisiasa kwa mawasiliano ya pande hizo mbili kwenye kipindi kijacho.

Bw. Blinken amesisitiza kuwa Marekani itaendelea kufuata sera ya China Moja, na inakubali kuwa Marekani na China zinapaswa kuendeleza uhusiano kwa msingi wa kuheshimiana, inapenda kudumisha mawasiliano na China, na kushughulikia tofauti zao kwa moyo wa uwajibikaji, ili kuepuka makabiliano na hata hatari ya kutokea mapambano.