Ubalozi wa Tanzania nchini China umetia saini makubaliano na kampuni ya JD.com ya China, ambapo Tanzania itaanzisha duka la kitaifa kwenye tovuti ya JD.com, na kuuza bidhaa zake bora kwa wateja wa China. Hii ni hatua nyingine ya China kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza mauzo ya bidhaa zao nchini China.
Katika miaka ya hivi karibuni, ili kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza mauzo ya bidhaa zao katika soko la China, China imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuondoa ushuru kwa zaidi ya asilimia 95 ya bidhaa za Afrika zinazoingia nchini humo, kuanzisha Maonesho ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika, kuzisaidia nchi za Afrika kushiriki kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Uingizaji Bidhaa ya China, na kuongeza nguvu ya kutangaza bidhaa za Afrika. Licha ya hayo, China pia imezisaidia nchi za Afrika kuongeza mauzo ya bidhaa zao nchini China kupitia makampuni yake ya biashara ya mtandaoni.
Mwaka jana, Balozi wa Rwanda nchini China James Kimonyo alijaribu kutangaza kahawa ya Rwanda kwenye tovuti ya Taobao.com iliyo chini ya Kampuni ya Alibaba ya China, ambayo ni jukwaa kubwa zaidi la mauzo ya bidhaa mtandaoni nchini China. Jambo lililomshangaza ni kwamba, ndani ya dakika chache, alifanikiwa kuuza mifuko yote 2,000 ya kahawa yenye uzito wa kilo 1,500 iliyoandaliwa.
Mwaka 2018, serikali ya Rwanda na Kampuni ya Alibaba ilizindua Jukwaa la Kimataifa la Biashara ya Mtandaoni eWTP, na kupitia jukwaa hilo, wakulima wa kahawa wa Rwanda wanaweza kuuza mazao yao kwa wateja wa China. Licha ya kuongeza mauzo, jukwaa hilo linalounganisha wakulima wa Rwanda na wateja wa China moja kwa moja, pia limeongeza kipato cha wakulima hao kwa dola nne kila wanapouza kilo moja ya kahawa.
JD.com ni moja ya kampuni kubwa zaidi za biashara kupitia mtandao nchini China, ina watumiaji waliojiandikisha zaidi ya milioni 700, na mauzo yake ya mwaka jana yalizidi dola bilioni 114.3 za kimarekani. Mwaka 2018, Kampuni hiyo ilianzisha Mradi wa maduka ya kitaifa ya nchi mbalimbali duniani. Maduka hayo yaliyoidhinishwa na serikali za nchi husika, yamekuwa jukwaa muhimu la kutangaza bidhaa za nchi za nje na kuongeza mauzo nchini China.
Kwenye hafla ya kusaini makubaliano hayo, balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki amesema Kampuni ya JD.com ya China ni jukwaa kubwa la manunuzi mtandaoni lenye watumiaji wengi, na ushirikiano na kampuni hiyo utaongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini China. Kampuni ya JD.com itashirikisha nchi nyingi zaidi za Afrika kwenye mradi wake wa maduka ya kitaifa, ili kuzisaidia kuongeza mauzo ya bidhaa zao nchini China, na kukidhi mahitaji ya wateja wa China.