Rais Xi Jinping atoa hotuba ya maandishi kwenye Mkutano wa Kilele wa COP26
2021-11-02 09:29:24| CRI

Rais Xi Jinping wa China ametoa hotuba ya maandishi kwenye mkutano wa kilele wa 26 wa Nchi zilizosaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26).

Kwenye hotuba yake, rais Xi amesema wakati athari hasi za mabadiliko ya tabianchi zimejitokeza siku hadi siku, hatua za pamoja zinahitajika kuchukuliwa sasa kuliko wakati wowote ule. Ametoa mapendekezo matatu: kwanza ni kutetea makubaliano ya pamoja, pili ni kuchukua hatua halisi, na tatu ni kuharakisha mageuzi ya kijani.

Rais Xi amesisitiza kuwa China itaendelea kufuata njia ya maendeleo endelevu ya kijani inayotoa kipaumbele katika uhifadhi wa mazingira, kuharakisha ujenzi wa mfumo wa uchumi wa kijani, kuendelea kusukuma mbele marekebisho ya muundo wa viwanda, kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kijani na kuongeza nguvu katika kuendeleza nishati endelevu. Amesema China inatarajia kuwa pande mbalimbali zitaimarisha mwitiko wao, na kuungana mkono katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ili kulinda maskani ya pamoja ya binadamu.