Watu wasiopungua 14 wauawa kwenye uvamizi wa kijambazi
2021-11-05 09:55:36| cri

Watu wasiopungua 14 wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa kwenye mapigano makali kati ya wezi wa mifugo na wafugaji kwenye eneo linalokabiliwa na vitendo vingi vya wizi wa mifugo katika kaunti ya Samburu, kaskazini mwa Kenya.

Kamishna wa kaunti ya Samburu Abdrizak Jaldesa alisema kuwa vifo vilivyoripotiwa ni kutoka pande zote mbili za wafugaji na majambazi na sasa kazi ya kusaka majambazi hao inaendelea. Mifugo takriban 1,000 imeibiwa katika uvamizi huo uliotokea Jumatano wiki hii, na mifugo iliyorejeshwa hadi sasa haijafikia hata asilimia 10.

Mapigano hutokea mara kwa mara katika sehemu hiyo ambako mifugo imekuwa chanzo kikuu cha mapato ya wakazi na wafugaji hubeba bunduki ili kulinda mifugo yao.