Mkuu wa jeshi nchini Sudan aamuru kuwaachia huru mawaziri wanne wa serikali ya mpito
2021-11-05 09:44:11| CRI

Televisheni ya taifa ya Sudan imesema, kamanda mkuu wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan ametoa amri ya kuwaachia huru mawaziri wanne wa serikali ya mpito iliyovunjwa hivi karibuni.

Maofisa hao walioachiwa ni pamoja na Waziri wa Mawasiliano Hashim Hasabal-Rasoul, Waziri wa Uchukuzi Ali Jiddo, Waziri wa Vijana na Michezo Yousif Adam na Waziri wa Habari Hamza Balol.

Mawaziri wengi wa serikali ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok walikamatwa Oktoba 25 kutokana na amri ya Al-Burhan.

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes anaongoza mazungumzo kati ya viongozi wa jeshi la Sudan na kundi la FFC ambalo ni muungano tawala wa vyama ili kumaliza mgogoro huo.

Wakati huohuo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres amemtaka mkuu wa jeshi la Sudan al-Burhan atafute utatuzi wa kisiasa wa mgogoro unaoendelea.

Katibu mkuu huyo amehimiza kuendelea na juhudi zote zinazolenga kutatua mgogoro huo wa kisiasa nchini Sudan, na kurejesha utaratibu wa katiba na mchakato wa mpito wa nchi hiyo.