China yasaidia Afrika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi
2021-11-09 14:33:08| CRI

China yasaidia Afrika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi_fororder_src=http___n.sinaimg.cn_sinakd20211104s_799_w1022h577_20211104_0b27-8c2dc277d012afb1dbe470f9f3a6c729.jpg&refer=http___n.sinaimg

Mkutano wa 26 wa Nchi Zilizosaini Makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) ulifanyika mjini Glasgow, Uingereza, na ulijadili masuala ya hali ya hewa yanayofuatiliwa na pande mbalimbali duniani.

Ikilinganishwa na maeneo mengine, bara la Afrika linaathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa. Katika miaka iliyopita, China imechukua hatua madhubuti katika ujenzi wa miundombinu, utafiti wa kisayansi, na mafunzo ya wafanyakazi ili kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na mabadiliko ya tabianchi duniani, majanga kama vile ukame, mafuriko na wimbi la joto kali yametokea mara kwa mara barani Afrika, na kusababisha kuongezeka kwa jangwa, mmomonyoko wa ardhi, kutoweka kwa viumbe na uhaba wa chakula. Wakati huohuo, kiwango cha maendeleo ya uchumi barani humo bado ni chini, hivyo ni vigumu kwa nchi za Afrika kukabiliana na changamoto hizo peke yao.

China na nchi za Afrika zimeshirikiana vizuri kwa miaka mingi katika kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabianchi. Kwa mfano, ushirikiano kati ya pande hizo mbili umepata mafanikio mazuri katika kuhimiza matumizi ya nishati safi. Katika miaka ya hivi karibuni, China imezisaidia nchi za Afrika kuendeleza matumizi ya nishati safi za jua, upepo, maji na jotoardhi kwa mujibu wa hali tofauti ya nchi zao, na kutekeleza miradi mingi mikubwa ya miundombinu ya nishati safi, ili kupunguza utoaji wa hewa inayoweza kuongeza joto na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Bwawa la Merowe nchini Sudan lenye urefu wa kilomita 9 limejengwa na kampuni ya China, na uwezo wake wa kuzalisha umeme unashika nafasi ya kwanza barani Afrika. Bwawa hilo limewanufaisha watu milioni 4 nchini Sudan, na kuboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wa nchi hiyo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Licha ya bwawa hilo, China pia imetekeleza miradi mingine mingi ya nishati mpya barani Afrika, ikiwemo Vituo vya Kuzalisha Umeme kwa Nishati ya Upepo vya De A nchini Afrika Kusini, Kituo cha Uzalishaji wa Umeme kwa Jotoardhi cha Okari nchini Kenya, na Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Nishati ya Jua cha Photovoltaic nchini Ethiopia.

Kwa upande wa utafiti, wanasayansi wa China wanatekeleza mradi wa kimataifa wa utafiti kuhusu mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya tafiti zao zinahusiana moja kwa moja na Afrika, kama vile athari ya mabadiliko ya tabianchi kwa maendeleo ya kilimo, rasilimali ya maji na usalama wa chakula katika Bonde la Mto Zambezi. Timu ya Utafiti wa Sayansi ya Mfumo wa Dunia ya Chuo Kikuu cha Tsinghua cha China imeanzisha ushirikiano na nchi nyingi za Afrika, na miradi yake ni pamoja na uchoraji wa ramani ya rasilimali za misitu ya mianzi katika nchi tatu za kusini mwa Afrika zikiwemo Kenya, Uganda na Ethiopia, ili kutafiti athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kukabiliana nazo.

Mbali na ujenzi wa miundombinu ya nishati safi na utafiti wa kisayansi, ushirikiano kati ya China na Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pia unahusisha ujenzi wa uwezo, na kuwafundisha wanasayansi vijana wa Afrika, jambo lenye umuhimu mkubwa sana kwa Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni, China imewapokea wanafunzi wengi kutoka nchi za Afrika wanaosomea sayansi ya asili nchini China, na wanafunzi hao watatumia ujuzi watakaoupata nchini China kusaidia Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa COP26, Rais Xi Jinping wa China amesema, pande zote zinapaswa kuimarisha hatua zao za kushirikiana katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi, na kufanya kazi kwa pamoja, ili kulinda sayari ya dunia ambayo ni makazi ya binadamu wote. Hivi ndivyo China ilivyosema, na pia ndivyo ilivyofanya!