Tanzania yaibuka kama kituo cha matibabu cha kikanda
2021-11-12 10:26:38| Cri

Tanzania imeibukia kama kituo cha matibabu cha kikanda, ikitoa huduma maalumu za afya. Dar es Salaam sasa imegeuka kuwa sehemu ya wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka nchi jirani.

Baada ya kupata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma ya afya katika miaka 60 iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza macho yake katika kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha utalii wa kimatibabu. Hili ni wazo la rais aliyepita hayati John Magufuli, ambaye mwezi Februari 2020 alianza kuongea kuhusu haja ya Tanzania kuwekeza dola bilioni 72 za Kimarekani kwenye kile alichokiita kama soko la utalii wa kimatibabu la kimataifa.

Mwezi Julai 2021, Dr Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alizindua timu ya kutangaza utalii wa kimatibabu. Dr Gwajima amesema serikali imetuma ombi kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO) ili Tanzania itambuliwe rasmi kama kituo cha utalii wa kimatibabu.